Wanawake wajawazito 200 wapatiwa msaada Vifaa wakati wa kujifungua.

Wanawake wajawazito 200 wapatiwa msaada Vifaa wakati wa kujifungua.

General / 18th November, 2022

Wanawake wajawazito wameshauriwa kuzingatia lishe bora inayoambatana na kufanya mazoezi mara kwa mara wakati wote wa ujauzito ili kulinda afya ya mama na mtoto itakayosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

 

Hayo yamesemwa leo Novemba 18, 2022 na Theodora Malala akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke Joketi Mwegelo katika uzinduzi wa mbio za Temeke Maternal Jogging zenye lengo la kuihamasisha jamii kuhusiana na uhusiano uliopo kati ya lishe bora wakati na baada ya ujauzito utakaosaidia kujenga kizazi bora.

 

Theodora ameishukuru Taasisi ya Hatua Group Afrika kwa kuwapatia vifaa vinavyotumika wakati wa kujifungua kwa kina mama wapatao 200 na kutoa wito kwa kina mama hao kuzingatia lishe bora pamoja na kufanya mazoezi hata baada ya kujifungua.

 

“Tunawashukuru sana na zawadi hizi tutaenda kuzitoa kwenu, tukiamini itakuwa ni kotisha ya kuendelea kukumbuka kwamba tulifanya jambo hili Fulani, siku Fulani katika hospitali ya Rangitatu ambayo itaturahisihia sisi tuwe tunakula vizuri, lakini vilevile tuzingatie mazoezi na tuhudhurie kliniki”. Amesema Theodora.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hatua Group Afrika  Derick Mgaya amesema taasisi hiyo ilianzisha programu ya Busela ili kutoa elimu kwa wanawake wajawazito juu ya namna bora ya kupata lishe bora, kuwahamasisha kufanya mazoezi pamoja na kuwapatia ushauri wa saikolojia.

 

Ameongeza kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuwafikia wanawake Zaidi ya elfu mbili huku lengo likiwa ni kuwafikia wanawake laki tatu nchini ifikapo 2024.

 

Sabrina Shabani ni miongoni mwa wanawake waliopata msaada huo ameishukuru Taasisi hiyo kwa kutoa msaada kwa kina mama wajawazito pamoja na elimu waliyopatiwa kuhusu umuhimu wa lishe bora.

Mbio hizo za Temeke Martenal Jogging zenye kauli mbiu isemayo ‘Ujauzito wenye Afya, Utoto wenye Afya’ zinatarajia kuanza Februari mwaka 2023.