Wakurugenzi wa Idara na Taasisi watakiwa kuongeza kasi kuhudumia wananchi

Wakurugenzi wa Idara na Taasisi watakiwa kuongeza kasi kuhudumia wananchi

General / 10th January, 2023



Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amewataka Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara kuongeza kasi ya kuwahudumia Wananchi hasa wawekezaji wa ndani na Nje ya Nchi kwani Wizara hio ndio mhimili wa uchumi wa Nchi hii.

Naibu Waziri Kigahe ameyasema hayo tarehe 9 Januari, 2023 katika ofisi ya Hazina ndogo Mkoani Morogoro alipofungua kikao kazi cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kujadili mkakati madhubuti wa utekelezaji wa majukumu na kubadilika kiutendaji ili kufikia adhma ya serikali ya awamu ya sita ya kuifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza la wawekezaji ili kuongeza ajira kwa watanzania kupitia sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil T. Abdallah ambaye ametoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri kuwa sehemu ya kikao kazi hicho ambacho kinaenda kuonesha dira na mwelekeo wa Wizara.

Dkt. Abdallah amesema kuwa lengo la kuwaleta pamoja wakuu wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ni kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini na kuja na mkakati madhubuti wa kiutendaji ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kikao kazi cha Katibu Mkuu kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Bw. Ally Gugu, Wakurugenzi wa Idara kutoka Wizara ya Uwkezaji, Viwanda na Biashara na Wakuu wa Tasisi zilizo chini ya Wizara.