Vijana 32,000 wapatiwa mafunzo ya kuwawezesha kujiajiri

Vijana 32,000 wapatiwa mafunzo ya kuwawezesha kujiajiri

General / 19th May, 2022

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia mfuko wake wa kuendeleza ujuzi imewapatia mafunzo mbalimbali vijana wapatao 32,000 nchi nzima ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.

Hayo yamesema na Meneja wa Miradi ya Elimu kutoka TEA ambaye pia ni  Mratibu wa Mfuko wa kuendeleza Ujuzi Masozi Nyirenda wakati akizungumza katika maonyesho ya wiki ya ubunifu yanayoendelea jijini Dodoma.

“Mfuko huu tulianza mwaka 2017/18 ambapo mpaka sasa vijana takriban 32,000 nchi nzima wameweza kupata mafunzo kupitia taasisi mbalimbali za mafunzo vikiwemo vyuo vikuu ,VETA,vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ,SIDO na taasisi nyingine za binafsi zinazoshiriki kutoa mafunzo kwa vijana.”amesema Nyirenda na kuongeza kuwa

“Mafunzo yameonyesha matokeo chanya kwani vijana wapatao asilimia 70  ya waliopata mafunzo wameweza kujiajiri na wengine wameweza kuajiriwa lakini na wengine waliojiajiri wameweza kuzalisha ajira kwa kuajiri wengine.”

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuwapata  vijana hao wa kuwapa mafunzo ,amesema wao wanatangaza ambapo  taasisi ambazo zipo tayari kutoa mafunzo zinaomba na baada ya hapo wanazijengea uwezo taasisi hizo ili zitoe mafunzo  yenye kuleta tija kwa vijana na Taifa kwa ujumla.

“Pia tunazipa taasisi hizo jukumu la kutangaza katika ngazi ya kaya na ngazi ya chini kabisa ili kualika wananchi waweze kupata mafunzo haya ambayo hutolewa bure  kwa wananchi kwa sababu tayari taasisi tumeshazijengea uwezo, kikubwa wananchi wanaposikia taarifa hii wao kazi kubwa ni kujitoa tu kwenda kuhudhuria mafunzo hayo ambayo hutolewa kwa muda mfupi kati ya wiki tano hadi miezi sita.”

Vile vile Nyirenda amesema TEA ina mfuko wa Elimu ambao kazi yake ni kufadhili miradi ya kuendeleza miundombinu,kutoa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na mazingira ya kufundishia katika shule za msingi sekondari mpaka vyuo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Miradi Mamlaka ya Elimu Tanzania Waziri Rajab amesema,wamekuja kwenye maonyesho hasa kuhusiana na kipengele cha ubunifu na ndio maana wamechukua baadhi ya wanufaika wa ufadhili wao katika eneo la ujuzi kuja kuonyesha kazi mbalimbali ambayo ni matokeo ya mafunzo waliyoyapata na namna yalivyowakwamua kutoka kwenye kutokuwa na ajira na kuwa na ajira.

“Kikubwa zaidi ufadhili tunaoutoa ni kuhakikisha vijana na akina mama wanaweza kupata mafunzo ili waweze kujiajiri wao wenyewe.”amesema Waziri