"Tumeongeza Bil.84" HESLB

"Tumeongeza Bil.84" HESLB

General / 21st November, 2022

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imethibitisha ongezeko la bajeti ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa asilimia 14.7 ikilinganishwa na kiasi kilichotengwa awali.


Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema kutokana na ongezeko hilo la fedha kwa sasa bajeti ya mikopo imefikia Sh654 bilioni kutoka Sh570 bilioni iliyotengwa hapo awali.


Kiasi hicho kitawezesha wanafunzi 28,000 kupata mikopo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa masomo na tayari fedha hizo zimeshafikishwa katika vyuo husika.


Hadi kufikia leo jumla ya wanafunzi 166,438 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh424.5 bilioni kati yao wa mwaka wa kwanza ni 68,460 na wanaoendelea ni 97,978.


Kulingana na Badru wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaolengwa kunufaika na mikopo hiyo kwa mwaka huu ni 71,000.


“Bajeti isingeongezwa ni wazi wanafunzi 28,000 wangekosa mikopo lakini kutokana na hatua hii iliyochukuliwa wataweza kupata ufadhili huu. Hawa waliopata walikuwa tayari wameshafanyiwa tathmini na kuonekana mahitaji yao ni makubwa,”amesema Badru.


Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson aliiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kufika mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ili kueleza sababu za kutoipa ushirikiano kamati ya Serikali iliyoundwa kuchunguza utaratibu wa kutoa mikopo kwa miaka mitano iliyopita.

Alisema kuhusu hoja kama HESLB inatoa mikopo sawa sawa itajadiliwa Februari mwakani wakati kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itakapokuwa inatoa taarifa yake bungeni na hivyo kuona kama kuna haja ya Bunge kuunda tume ya kuchunguza bodi hiyo ama la.


Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, (HESLB), inahitaji Sh800 bilioni ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa kujiunga na vyuo vikuu.