Tanzania yapokea mkopo wa Trilioni 1.2 kutoka Benki ya Dunia

Tanzania yapokea mkopo wa Trilioni 1.2 kutoka Benki ya Dunia

General / 22nd November, 2022


Serikali imethibitisha rasmi kuanza utekelezaji wa Mradi wa Bonde la Msimbazi Aprili 2023.

Hatua hiyo imethibitishwa wakati wa utiaji saini kati ya Serikali na Benki ya Dunia inayotoa mkopo wa riba nafuu dola 535milioni, sawa na Sh1.2 trilioni.

Katika makubaliano hayo, Serikali imepokea mkopo kwa ajili ya miradi miwili: mkopo wa dola 335 milioni (Sh777.17 bilioni) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini chini ya  Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) na dola 260milioni (463.98 bilioni) kwa ajili ya mradi wa bonde hilo.

Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema; “kati ya hizo dola 260milioni, kuna dola 30milioni msaada kutoka Uholanzi na mkopo wa dola 30 milioni kutoka Hispania, tunawashukuru sana.”

"Mikataba hii miwili yenye thamani ya dola milioni 535 sawa na Sh trilioni 1.24 itaandika historia na kukuza uchumi wa nchi.Na hapa nieleze kwamba huu ni mwanzo tu kati ya yale mambo makubwa yanayokwenda kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.Kwa mwaka huu wa fedha anakwenda kufanya ujenzi wa miradi itakayoandika historia."



Akizungumza kuhusu miradi hiyo Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema daraja la kisasa linalokwenda kujengwa Jangwani muonekano wake utakuwa kama daraja la Tanzanite ambalo linapita katika Bahari ya Hindi au daraja la Kigamboni.

" Ujenzi wa daraja hili utakapokamilika unakwenda kuondoa kabisa mafuriko ambayo yamekuwa yakisababidha adha kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.Ujenzi wa daraja la Jangwani utakuwa daraja la mita 390 na litainuka kwa mita sita.Pia ujenzi utahusisha upanuzi wa mto kwa kilometa 1.8 chini, kutakuwa kingo za zege,"amefafanua.

“Ujenzi utagharimu zaidi ya dola milioni 63.3 na hivi karibuni tunatarajia kutangaza tenda ambapo baada ya miezi mitatu hatua za awali zitakuwa zimekamilika,”amesema na kuongeza usanifu wa ujenzi tayari umekamilika na ujenzi utakamilika baada ya miaka mitatu.