Sumu kuvu tishio la usugu wa Dawa kwa Binadamu na Mifugo

Sumu kuvu tishio la usugu wa Dawa kwa Binadamu na Mifugo

Health and Relationships / 14th February, 2022


Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 inatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na mifugo.

Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.

Dkt. Bitanyi amesema wakala hiyo inatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.

Katika hatua nyingine mtendaji mkuu huyo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ametoa wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.

Amebainisha kuwa matumizi ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili, vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.

Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua ubora wa vyakula vya mifugo katika Wilaya za Temeke na Ubungo, Afisa Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA Dkt. Evaline Mfuru amesema uwiano sawa wa virutubisho vinavyotakiwa kwenye vyakula vya mifugo kwa kiasi kikubwa hupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Nao baadhi ya wafugaji na wazalishaji wa vyakula vya mifugo wamesema zoezi la uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo litakuwa na tija kwa kuhakikisha vinapatikana vyakula bora, ambavyo vitaleta tija kwa mfugaji pamoja na kuondoa sokoni vyakula vya mifugo ambavyo havikidhi vigezo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta tija kwa mfugaji.