Serikali kulipa Bilioni nne za ATCL kwenye mifuko ya hifadhi za jamii

Serikali kulipa Bilioni nne za ATCL kwenye mifuko ya hifadhi za jamii

General / 6th February, 2023

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema licha ya kutokuwepo kwa madeni mapya tangu kufufuliwa kwa Shirika la Ndege la ATCL, Serikali katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya kulipa deni la Shilingi Bilioni 4 inayotokana na kutokuwasilisha kwa michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi za jamii.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Atupele Mwakibete leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Anjelina Malembeka aliyataka kujua ni lini Wastaafu wa ATCL watalipwa fedha zao.

"Kabla ya kuanza kwa juhudi za ufufuaji wa ATCL , Septemba mwaka 2016 ATCL ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za uendeshaji kwa kukosa mtaji, kuwa na ndege mbovu, kushindwa kulipa madeni ya wazabuni, kutowasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko ya  hifadhi za jamii,"

"Fedha za kulipa madeni hayo zimetengwa katika bajeti ya 2022/2023 , hivyo madeni hayo ya michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi za jamii yatalipwa katika mwaka huu wa fedha" Amesema Mhe. Mwakibete.

Aidha Mwakibete ameeleza mikakati ya serikali katika kuzuia madeni mapya katika Shirika hilo.

" Serikali imejipanga kuzuia ama kutozalisha madeni mengine , hadi sasa tangu mwaka 2016 tumekuwa tukilipa wafanyakazi wote na hakuna deni jipya,  lakini kwenye mwaka wa fedha huu 2022/23 tumetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 10 ili kulipa wafanyakazi wote waliokuwa wa ATCL kama deni la nyuma". Amesema Mwakibete.

Katika hatua nyingine Mhe. Mwakibete amesema kwa sasa kuna takribani Marubani 106 huku kati yao wanawake 11 na wanaume wakiwa ni 95.