Sekta Binafsi yaendelea kutajwa kukuza uchumi wa Taifa

Sekta Binafsi yaendelea kutajwa kukuza uchumi wa Taifa

General / 2nd February, 2023

Serikali imeendelea kuibeba sekta binafsi na kutambua mchango wake na kuhakikisha mchango huo unaongezeka katika kukuza pato la taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji leo Februari 2, 2023 katika Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na sekta Binafsi wenye kauli mbiu " Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa maendeleo ya Uchumi wa Tanzania " uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Unapoongelea pato la taifa lazima tuanzie pato la mtu mmoja mmoja , kwa sababu pato hili ndilo linabeba pato la taifa, Sekta binafsi ndiyo inaajiri kwa kiwango kikubwa vijana wetu na watanzania kwa ujumla," Amesema Dkt. Kijaji.

"Sekta binafsi ndiyo inayolipa kodi kubwa , ndiyo inayoendesha Taifa lolote lile duniani, hivyo kwa kutambua hayo yote, Mhe. Dkt. Samia ameamua kuibeba sekta binafsi kwenye safari mbalimbali lakini kwenye vikao mbalimbali katika nchi yetu" Ameongeza Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji amesema licha ya uchumi wa Dunia kutetereka , Tanzania imeendelea kuimarika kutokana na kuendelea kutafuta mbinu za kuboresha  mazingira ya biashara na uwekezaji kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema katika uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini Serikali imeendelea kutekeleza sheria, sera na mipango mbalimbali kwa ustawi wa Sekta binafsi.

"Kupitia utekelezaji huo, Sekta binafsi itaweza kuzalisha bidhaa, zinazokidhi masomo ya ndani na nje ya nchi , kufanya biashara kiushindani katika mazingira rafiki na kuchangia Uwekezaji  na viwanda nchini kwetu" Amesema Bw. Gugu.