NBC yapongezwa kustawisha sekta ya Viwanda nchini

NBC yapongezwa kustawisha sekta ya Viwanda nchini

General / 20th November, 2022

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imepongezwa kwa juhudi na mchango mkubwa katika kustawisha sekta ya Viwanda nchini kutokana na huduma za kifedha zinazosaidia kuongeza ufanisi wa uzalishaji nchini.


Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za 16 za Rais kwa vinara wa Uzalishaji viwandani (PMAYA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam huku akisema mchango wa taasisi za kifedha ni muhimu katika kukuza sekta ya viwanda na kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya nchini.

“Kama ambavyo wadau wenyewe wa sekta ya viwanda wanavyowaita Benki ya NBC mshirika muhimu wa sekta ya Viwanda nami pia kwa niaba ya serikali nawapongeza NBC pamoja na wadau wengine wote kwa kuwa pamoja na sekta hii muhimu.’’

“Mchango wenu ni muhimu sana ninaomba sana ushirikiano huu uendelee zaidi kwasababu sekta ya viwanda inategemea zaidi huduma nzuri za kifedha…hongereni sana NBC,’’ Amesema Dkt. Mpango

Awali akizungumza kwenye hafla ya tuzo hizo zilizoratibwa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi alisema mafanikio makubwa ambayo benki hiyo inayapata kwa kiasi kikubwa yanachagizwa na dhamira thabiti pamoja na jitihada za serikali katika kujenga Tanzania inayoondeshwa na uchumi wa Viwanda na Biashara.

“Ushiriki wa Benki ya NBC kwenye matukio kama haya yanayowakutanisha wadau wa sekta ya viwanda nchini yanatupa ufahari sana kwa kuwa yanatukutanisha na wadau wetu muhimu wote tukiwa na dhamira moja kuu ambayo ni kuongeza ukuaji wa uchumi na ushindani wenye tija kwa faida ya taifa letu. Tunawashukuru sana Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) kwa kutuona NBC kama wadau sahihi katika kufanikisha tuzo hizi muhimu,’’

Kwa mujibu wa Bw Sabi, kupitia uwekezaji mkubwa katika huduma za Kidigitali, benki hiyo kwasasa imefanikiwa kurahisisha utoaji wa huduma zake kwa wateja wote wakiwemo wamiliki wa viwanda ambao kwasasa hawalazimiki kutembelea matawi ya benki hiyo ili kupata huduma kwa kuwa wanaweza kukamilisha huduma zote muhimu za benki hiyo wakiwa kwenye biashara zao kupitia huduma za kidigitali.

Katika hatua nyingine Sabi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau hao wa viwanda kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kuwekeza kwenye Hati Fungani ya NBC Twiga Bond ili waweze kunufaika na faida mbalimbali zitokazo na Hati fungani hiyo.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango (wa pili kulia) akikabidhi cheti cha utambuzi kwa uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi (wa pili kulia) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo kufanikisha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini katika Tuzo za 16 za Rais kwa vinara wa Uzalishaji viwandani (PMAYA) zilizoratibiwa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI). Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.