Mgodi watozwa faini Sh1 bilioni

Mgodi watozwa faini Sh1 bilioni

Business / 25th April, 2022

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeitoza faini ya Sh1 bilioni mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara baada ya kupasuka kwa bomba katika kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime.

 

Pia Waziri wa Madini, Doto Biteko amemuondoa katika nafasi yake ofisa mgodi mkazi, Hamad Kallaye kwa madai ya kushindwa kutimiza wajibu wake.

 

Akizungumza baada ya kufika katika eneo hilo leo Jumapili Aprili 24, 2022, Biteko amesema kupasuka kwa bomba hilo limetokana na uzembe wa uongozi wa mgodi huo.

 

" Maji yamevuja kwa zaidi ya saa nne bila kuchukua hatua zozote wakati hapa mtu akiingia na kuiba atapatikana ndani ya nusu saa tu hivi kama haya maji yangekuwa na sumu leo tungekuwa tunaongea lugha gani" amesema Biteko

 

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka amesema lengo la adhabu hiyo inayotakiwa kulipwa ndani ya siku 14 imetolewa kwa lengo la kuonya ili mgodi huo uzidishe umakini katika kazi zake.

 

NEMC imesema bomba hilo lililopasuka linatoa maji katika bwawa linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ya mashimo ya dhahabu kwenye mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara na si kwenye bwawa la sumu kama ilivyodhaniwa awali.

 

Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa, Jerome Kayombo amesema lipo bwawa maalum linalokusanya maji  yanayotiririka kutoka kwenye miamba kwa ajili ya kuhifadhiwa  kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya kutibiwa na kutumika kwa matumizi ya kawaida.

 

" Lipo bwawa maalum linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ambayo kwa asili yana tindikali kwahiyo yakishajaa kwenye bwawa yanasafirishwa kwenye mfumo kwa ajili ya kutibiwa ili kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya kawaida," amesema

 

Amesema kuwa mara baada ya tukio hilo kutokea,  juzi wataalam kutoka NEMC  walifika katika eneo hilo na tayari wamechukua sampuli za maji kutoka katika maeneo tofauti ikiwemo kwenye mto Tigite  ili kupima ubora wa maji hayo.

 

Naye Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Musa Kazimila amesema vipimo vya awali vinaonyesha  maji katika eneo hilo ni salama, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea na majibu yanatarajiwa kutoka Jumatano Aprili 27, 2022.

 

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally lly Hapi amesema Serikali ya mkoa itaweka utaratibu maalum wa kulinda maeneo ambayo ni hatarishi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

 

Kwa upande wake Meneja wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko amesema baada ya kupata taarifa za kupasuka kwa bomba hilo walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi ili kuzuia hali hiyo.