Mfumo wa kielektroniki wa taarifa za pamoja waanzishwa na TIC kuhudumia wawekezaji

Mfumo wa kielektroniki wa taarifa za pamoja waanzishwa na TIC kuhudumia wawekezaji

General / 4th August, 2022

Bw. Venance Mashiba Meneja wa Kanda wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Nyanda za juu Kusini akitoa maelezo kwa Jaji James Karayevala Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya wakatialipotembelea banda la Kituo cha Uwekezaji TIC katika maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya. 

Jaji James Karayevala Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya akimweleza jambo Bw. Venance Mashiba Meneja wa Kanda wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Nyanda za juu Kusini wakati alipotembelea katika banda hilo.

……………………………………

Kituo cha Uwekezaji nchini TIC kimeanzisha mfumo wa kielekroniki wa taarifa za pamoja kutoka taasisi mbalimbali kumhudumia mwekezaji ili kutoa huduma bora na haraka katika dawati moja la kituo cha (TIC) yaani huduma za mahala pamoja ili kurahisisha huduma kwa wawekezaji wanapotaka kuja kuwekeza nchini. 

Huduma hizo zote ili uzipate awali ilitakiwa ni lazima uende katika taasisi mbalimbali ambazo ziko maeneo tofauti jambo ambalo limekuwa linawapa usumbufu wawekezaji wanapokuwa wanafuatilia huduma mbalimbali katika taasisi zinazohusika ili kuwekeza nchini.

Akizungumza leo katika Maonesho ya Kilimo-Nane Nane yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale mkoa wa Mbeya Bw. Venance Mashiba Meneja wa Kanda wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Nyanda za juu Kusini amesema Umeanzishwa mfumo wa pamoja wa kielektroniki unaotumia teknolojia ya mawasiliano.

“Hivyo taasisi zote zinaunganisha mifumo yake ya utoaji hudumana kuwa katika mtandao mmoja ili mwekezaji anapokuja kwenye eneo moja kama vile (TIC) ataanzisha mahitaji yake ya uwekezaji kwa kuongea na (TIC) hivyo taarifa zake zitaenda kwenye taasisi zingine mbalimbali  kama vile BRELA, Uhamiaji, TRA, TBS, Wizara ya Viwanda na maeneo mengine bila yeye kutoka pale alipo,”. Amesema Bw. Venance Mashiba

Ameongeza kuwa mwekezaji atafanya maombi yake kupitia mtandao na taarifa zake zitahama kwenda kwenye taasisi zingine kisha mwekezaji anapata huduma aliyoitarajia bila kwenda kwenye taasisi husika.

Aidha amebainisha kwamba mfumo huo umeshakamilika na sasa unafanyiwa majaribio ya ndani ili kuuthibitisha kama umeshaweza kufanya kazi vizuri ili kutolewa nje uanze kufanya kazi ndiyo maana tumekuja kuutangaza hapa ili wawekezaji wauelewe na utakapoanza waweze kuutumia vizuri.

Aidha Bw. Venance Mashiba amesema lengo lingine la kushiriki katika maonesho hayo ni kutangaza fursa zilizopo katika ukanda wa nyanda za juu kusini ambazo ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi  kwenye mnyororo mzima wa thamani ya uwekezaji kwenye kilimo kama vile utengenezaji wa mbolea, kilimo cha mazao mbalimbali usindikaji na uchakataji wa mazao,Ufugaji wa mifugo na usindikaji wa bidhaa zake lakini pia Madini, Majengo, Elimu na fursa zingine nyingi.

Amewahimiza wananchi kutembelea kwa wingi katika banda la taasisi hiyo ili kupata elimu mbalimbali inayotolewa bandani hapo kuhusu shughuli mbalimbali za kuhudumia wawekezaji lakini pia kujua fursa mbalimbali zilizopo katika ukanda wa Nyanda za juu kusini mikoa ya Mbeya , Iringam Ruvuma, Songwe na katavi.