Marufuku magari yanayosafirisha abiria usiku bila vibali

Marufuku magari yanayosafirisha abiria usiku bila vibali

General / 25th April, 2022

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabaranii, Wilbroad Mutafungwa, amewaonya wamiliki na madereva wa mabasi madogo aina ya Coaster wanaofanya safari usiku kinyume na utaratibu akiwataka kuacha mtindo huo.

 

Amesema vitendo vinahatarisha usalama wa madereva na watumiaji wengine wa barabara, pia vinachangia ongezeko la ajali barabarani.

 

Onyo hilo amelitoa leo Aprili 25, 2022, mbele ya waandishi wa habari huku akiwataka wamiliki namadereva hao kufuata sheria ikiwemo kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra).

 

"Kwa siku za hivi karibuni kumeibuka vitendo vya usafirishaji abiria usiku kwa kutumia magari hayo bila kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwa na vibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra)," amesema.

 

Mutafungwa amebainisha kuwa safari hizo huanzia katika vituo ambavyo si rasmi hasa nyakati za jioni kuelekea mikoa mbalimbali.

 

Ametaja safari hizo huanzia Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Shinyanga, Mbeya, Moshi na Arusha na kwamba Coaster hizo alidai zinajulikana kwa majina ya 'mchomoko' au 'hakuna kulala'.