Mabalozi wa Tanzania wakabidhiwa Vitabu kufundisha Kiswahili nje ya nchi

Mabalozi wa Tanzania wakabidhiwa Vitabu kufundisha Kiswahili nje ya nchi

General / 21st November, 2022

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake Said Yakubu imekabidhi vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa Mabalozi wa Tanzania kwa ajili ya kufundishia lugha ya kiswahili nje ya nchi kwenye hafla ya mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania ulioanza Novemba 14, 2022.

Akizungumza wakati akitoa mada kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Ubidhaishaji wa Lugha ya Kiswahili kwa mabalozi wa Tanzania na Watumishi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Naibu Katibu Mkuu Said Yakubu amesema mabalozi wana nafasi kubwa ya kukuza na kukiendeleza kiswahili katika nchi wanazoziwakilisha na kupitia mpango huo utawasaidia kujua njia zitakazosaidia kukuza lugha ya kiswahili.

Amesema kiswahili kwa sasa kina wazungumzaji takribani milioni 500 na vituo takribani 150 vinavyofundisha lugha hiyo ambapo watanzania 2000 wamepata ajira za kuweza kufundisha katika vituo hivyo. Huku akisema hiyo ni dalili kwamba kiswahili kinakubalika duniani na kinakuwa kwa kasi.

Ameongeza kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa bungeni alisema ili kukuza kiswahili balozi zote zijenge vituo vya kufundishia kiswahili ili iwe nguzo ya kujenga diplomasia ya uchumi na Watanzania na kuongeza wigo wa watumiaji wa kiswahili duniani.

Naye Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi amesema mkakati huo ni wa miaka 10 na unatarajiwa kutekelezwa kati ya mwaka 2022-2032.

Katika Hafla Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekabidhi Tuzo kwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Samwel Shelukindo kwa kutambua mchango wake katika kukuza na kueneza kiswahili.