Ludovick Utouh alia na Katiba

Ludovick Utouh alia na Katiba

General / 17th May, 2022

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amependekeza kufutwa kwa baadhi ya vipengele katika Katiba ya nchi, ili kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.

 

Amependekeza kufutwa kwa Ibara ya 90 (2)(b) kwenye Katiba, ili kuongeza usimamizi wa fedha za umma, kwa kuwa ibara hiyo inayomruhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulivunja Bunge iwapo halitoridhia Bajeti ya Serikali, ili kuitisha uchaguzi mkuu mwingine, hii inawafunga midomo wabunge wengi, kwani wengi hawako tayari kurudi kwenye uchaguzi.

 

“Ibara hii inalibana Bunge kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali. Inawatisha wabunge, hivyo kupitisha hata bajeti isiyo na uhalisia. Wabunge hushika shilingi, lakini huiachia kwa kuogopa kurudi kwenye uchaguzi. Wajibu tunapendekeza ibara hii ifutwe kwenye Katiba ya nchi yetu,” alisema Utouh.

 

CAG huyo mstaafu alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano ulioikutanisha taasisi ya Wajibu inayosimamia uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma na waandishi wa habari kujadili yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG kwa mwaka 2020/21.

 

Utouh alikazia hoja hiyo wakati ofisa wa Wajibu, Jackson Mmari alipokuwa akitoa majumuisho na mapendekezo ya taasisi hiyo kuhusu ukaguzi uliofanywa na CAG.

 

“Kwa ujumla, Wajibu tunaona kuna rampant mismanagement of public funds (matumizhi mabaya ya fedha za umma). CAG amebaini viashiria vya rushwa katika matumizi ya zaidi ya Sh3.365 trilioni, kuna kampuni amekuta inachimba madini hifadhini kinyume na utaratibu,” alisema Mmari.

 

Mkaguzi mkuu wa ndani

 

Eneo jingine aliloweka msisitizo Utoah ni kutaka mkaguzi mkuu wa ndani wa hesabu za Serikali ahamishwe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwenda ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.

 

Kwa kuzingatia ukweli kwamba mkaguzi mkuu wa ndani anawajibika kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, hivyo wigo wake wa kushauri unakuwa umebanwa, suala linaloinyima Serikali nafasi ya kushauri vema zaidi.

 

“Iwapo mkaguzi mkuu wa ndani atakuwa chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, atakuwa na wigo mpana wa kupokea ripoti kutoka kwa wakaguzi wa ndani wa halmashauri, taasisi na mashirika ya umma, hivyo kuishauri Serikali mapema. Ripoti yake itakuwa inatoka mapema kabla ya ile ya CAG, hivyo Serikali itapata muda mwingi wa kurekebisha na kufuatilia kasoro zilizopo,” alisema CAG Utouh.

 

Kwa sasa, alisema mkaguzi mkuu wa ndani anamkagua mlipaji mkuu wa Serikali na ripoti ya ukaguzi huo anamkabidhi mlipaji huyo aliyemkagua, jambo linalomnyima uwezo wa kumwonyesha udhaifu uliopo kwenye taasisi anayoisimamia.

 

 

 

Rais kushinda tuzo

 

Pia Utouh alionyesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa Rais wa Tanzania kushinda tuzo za uongozi bora kutoka taasisi za kimataifa, mfano Mo Awards akisema Katiba inamnyima nafasi hiyo.

 

Mkaguzi huyo alisema ibara ya Katiba inayosema Rais hawezi kushtakiwa kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani, inamnyima mkuu huyo wa nchi nafasi ya kuchukua tahadhari kwa kila anachokifanya, kwani anajua hawezi kuchukuliwa hatua.

 

“Hata Rais wa Tanzania afanyeje, hiki kifungu hakiwezi kumpa tuzo. Ukiangalia kwa umakini, utagundua wengi huwa wanajisahau wakiwa kwenye muhula wa pili. Wanapunguza umakini kwa kiasi fulani,” alisema Utouh.

 

Mapendekezo mengine yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa fedha za umma, Mmari alisema ni sheria ya ununuzi wa umma itoa adhabu kwa maofisa husika wanaopindisha utaratibu na uwepo mkakati madhubuti ya kupambana na vihatarishi vya rushwa katika matumizi ya fedha za umma.

 

Wajibu pia imemshauri CAG kuangalia mambo mengine licha ya kukagua taarifa za fedha tu, ili kutanua ukubwa wa ripoti yake. Taasisi hiyo imeshauri hivyo licha ya ukweli kwamba CAG hukagua ufanisi wa miradi na mifumo ya umma inayotumika maeneo tofauti.

 

Vilevile, imesema Serikali iitumie mifumo ya utekelezaji wa ripoti ya CAG ambayo kwa muda mrefu imefungwa, lakini haifanyiwi kazi. Mmari pia alisema, “wananchi wapewe taarifa za matumizi ya rasilimali za Taifa.”

 

 

 

Wadau watia neno

 

Kuhusu hoja ibara ya Katiba, Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo alisema inastahili kurekebishwa kama si kuondolewa kabisa, kwani inawanyima wananchi fursa ya kuzisimamia vema rasilimali zao.

 

“Katiba inatakiwa itoe uhuru mkubwa wa wananchi kusimamia rasilimali zao, hii ibara haifanyi hivyo,” alisema Lyimo.

 

Kuhusu hoja hiyo, Rais wa TAA, Lyimo alisema inaangukia kwenye utawala bora, suala wanalijadili na kulisisitiza kila wakati miongoni mwa wahasibu na menejimenti.

 

“Kwenye kampuni na mashirika ya kimataifa, mkaguzi mkuu wa ndani anaripoti kwa bodi ya wakurugenzi ingawa kikawaida hufanya kazi na mkurugenzi wa fedha. Hili likiingizwa serikalini nako itasaidia kuongeza utawala bora. Hata kama sio kwa katibu mkuu kiongozi, ila isiwe kwa katibu mkuu. Inaweza ikawa kamati inayohusika na utawala bora,” alipendekeza Lyimo.

 

Kwa ngazi za chini mfano halmashauri, Lyimo alisema mkaguzi wa ndani anaweza kuripoti kwa baraza la madiwani na inaweza ikafanywa kwa namna nyingine yoyote ila isiwe kwa mkuu wake anayeweza kumwadhibu kutokana na utendaji wa kila siku.

 

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara alisema ajenda ya kubadili Katiba ya nchi ni ya vyama vya upinzani, kwani chama tawala kwa sasa kinatekeleza ilani iliyoinadi kwa wananchi.

 

“Uchaguzi uliisha mwaka 2020, tukirudi mwaka 2025 wananchi hawatotuuliza kuhusu Katiba kwa sababu hatukuwaahidi kuibadilisha,” alisema Waitara.

 

Kuhusu upitishaji wa bajeti, alisema haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania Bunge lisiipitishe. Na kwa hii inayoendelea kujadiliwa ambayo jimbo lake limetengewa Sh1.1 bilioni kujenga barabara vijijini, Sh2.4 bilioni kujenga madarasa na zaidi ya Sh2 bilioni kusambaza maji kwa wananchi itakuwa ngumu kwa mbunge kuikataa.

 

“Kila jimbo limetengewa fedha za miradi. Ukiikataa maana yake hutaji hivyo vitu vifanyike kwenye jimbo lako. Bunge litaweza kuikataa bajeti kikitokea kitu cha ajabu, mfano mawaziri kujiongezea mishahara na safari za nje ila kama fedha zinarudishwa kwa wananchi, hakuna atakayepinga,” alisema Waitara.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben alisema mambo yanayogusa Katiba yanahitaji mjadala wa kitaifa kupata mwafaka wake.

 

“Kukiwa na malalamiko mengi ya wananchi, basi Katiba nzima inaweza kubadilishwa lakini yakiwa machache, ibara yenye mapungufu inaweza kurekebishwa,” alisema Rose.

 

 

 

Serikali yafafanua

 

Akizungumzia upitishaji wa bajeti, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema haoni tatizo la ibara hiyo ya Katiba kwa Bunge kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

 

“Rais atalivunja Bunge iwapo litashindwa kuisimamia na kuishauri Serikali. Katika kuisimamia Serikali, Bunge huonyesha udhaifu wowote uliopo, baada ya hapo linatakiwa lishauri cha kufanya kuboresha hali iliyopo. Likishindwa kufanya haya yote mawili ndipo Rais anaweza kulivunja, ili atafute watu wengine watakaomsimamia na kumshauri. Rais ni mwakilishi wa wananchi,” alisema Tutuba.

 

Hata akilivunja Bunge, Tutuba alisema Rais anayo mamlaka ya kuidhinisha theluthi moja ya kiasi kilichopendekezwa, ili shughuli za Serikali ziendelee kutekelezwa kama kawaida wakati uchaguzi mkuu ukirudiwa.

 

Kuhusu mkaguzi mkuu wa ndani kuripoti kwa katibu mkuu kiongozi au kamati ya utawala bora, alisema hakuna nchi yoyote duniani inayotumia mfumo huo.

 

“Ukimtoa kwangu, huyo hawi tena mkaguzi wa ndani. Atakuwa sawa na CAG kwa hiyo tutakuwa na ma-CAG wawili,” alisema Tutuba.

 

Kwa utaratibu uliopo, alisema wakaguzi wa ndani 528 waliopo kwenye halmashauri, taasisi na mashirika ya umma wanafanya kazi kubwa ya kuishauri Serikali na kiasi kikubwa cha hoja zinazoibuliwa na CAG huanzia kwao.

 

“Asilimia 70 ya hoja za ripoti ya CAG ya mwaka jana zilianzia kwa wakaguzi wa ndani. Hoja zao huwa zinafanyiwa kazi kama kawaida,” alisema Tutuba.