Kuelekea Uzinduzi wa TTMOA, wataja mafanikio Miradi ya Kimkakati
Na Rajabu Msangi
Chama cha Wamiliki wa Matipa na Mashine Tanzania (TTMOA)
kimesema kimefanikiwa katika kujumuisha sehemu kubwa ya maudhui ya ndani hasa
katika miradi mikubwa na ya kimkakati ya maendeleo ikiwemo kusambaza vifaa na
mashine.
Hayo yamebainishwa leo 18 Novemba 2022 na Mwenyekiti wa Chama hicho Emmanuel Moshi
wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Onomo jijini Dar es
Salaam ikiwa ni kuelekea uzinduzi wa Chama hicho cha TTMOA unaotarajiwa
kufanyika Novemba 25, 2022.
“Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la
Julius Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam mpaka Mwanza,
Miradi mbalimbali ya Mamlaka ya Barabara nchini (TANROAD) tumekuwa tukishiriki
moja kwa moja kupeleka vifaa kwa wakandarasi na kwenye sekta ya madini hasa
katika makaa ya mawe ambayo ni malighafi inayotafutwa sasa tumeshiriki pia”
Amesema Bw. Moshi.
Aidha Bw. Moshi amesema TTMOA ni chama cha biashara ambacho
kimeanzishwa tangu mwaka 2018 kikiwa na lengo la kuwawakilisha na kutetea
maslahi ya wafanyabiashara wa Tipa na Wamiliki wa Mitambo hapa nchini.
“Lengo ni kupitia sera yenye msingi wa ushahidi, utafiti
katika utetezi na ushawishi tukifanya kazi na Serikali kwa niaba ya wanachama
wetu” Amesema Bw. Moshi.
Uzinduzi wa Chama hiki
cha Wamiliki wa Matipa na Mashine Tanzania (TTMOA) utafanyika Novemba 25, 2022
katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete kama Mgeni rasmi katika uzinduzi
huo.