KNAUF Tanzania Kuwekeza Bilioni 115 upanuzi kiwanda Mkuranga

KNAUF Tanzania Kuwekeza Bilioni 115 upanuzi kiwanda Mkuranga

General / 21st November, 2022

Mkurugenzi  Mtendaji wa Kampuni ya Knauf Gypsum Tanzania inajishughulisha na utengenezaji na uuzaji wa vifaa vya ujenzi  Ilse Boshoff (kulia) na meneja masoko wa kampuni hiyo Lilian Mangaru (kushoto) wakimkabidhi mkurugenzi wa kampuni ya  Super Terrazzo Ltd Nish Hiran tuzo baada ya kuibuka mshindi  wa usambazaji wa bidhaa za kampuni hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam .



Kampuni inayojishughulisha na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi ya Knauf Gypsum Tanzania imesema mazingira ya uwekezaji hapa nchini yameboreka kwa kiasi kikubwa na kutangaza kuwekeza shilingi bilioni 115 katika upanuzi wa kiwanda chake kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.

Kampuni hiyo yenye asili ya Ujerumani tayari imeshawekeza kiasi cha shilingi bilioni 163 hapa nchini kwenye kiwanda na uzalishaji wa vifaa mbali mbali vya ujenzi wa nyumba ikiwamo gypsum na imesema itawekeza kiasi kingine cha shilingi bilioni 115 kufikia mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa halfa ya chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili ya kuwashukuru wateja wake na wadau mbalimbali, Mkurugenzi wa Knauf ukanda wa Afrika Mashariki Ilse Boshoff ameishukuru serikali, wateja na wadau mbali mbali kwa kuifanya safari ya uwekezaji wa kampuni hiyo hapa Tanzania yenye mafanikio.

“Kila kunapokucha kampuni ya Knauf inapiga hatua kadhaa mbele. Historia yetu kwa hapa Tanzania ilianza mwaka 2014 tulipofungua ofisi na baadaye kuanzisha Kampuni ya Knauf Gypsum Tanzania na kuanza kazi rasmi mwaka 2017,” alisema.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa mwaka 2018 kampuni hiyo ilianza ujenzi wa kiwanda cha kisasa kilichopo Mkuranga mkoani Pwani na mwaka 2020 kilianza uzalishaji kikiwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba milioni 15 kwa mwaka.

Akitangaza uwekezaji zaidi katika kiwanda hicho alisema.,“Uwezo wa uzalishaji kwa kiwanda cha Mkuranga ni mita za mraba milioni 15 kwa mwaka na malengo yetu ni kukipanua na kukiwezesha kuzalisha mita za mraba milioni 43 kwa mwaka kufikia mwaka 2025. Uwekezaji huu utagharimu shilingi bilioni 115,”