Faida ya filamu ya Royal Tour

Faida ya filamu ya Royal Tour

Business / 18th April, 2022

Viongozi wa sekta mbalimbali nchini wameeleza namna Tanzania itakavyonufaika kutokana filamu ya ‘Royal Tour’ itakayozinduliwa kesho na Rais Samia Suluhu Hassan jijini New York nchini Marekani.

 

Filamu ya Royal Tour iliyorekodiwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar ina lengo la kutangaza duniani vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

 

Royal Tour ilianza kurekodiwa Agosti 29, 2021 na muongozaji wa filamu hiyo ni Peter Greenberg aliyeambatana na Rais Samia kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Mji Mkongwe na hifadhi za Taifa zinazopatikana Tanzania bara.

 

Viongozi hao wakiwemo mawaziri wa utalii wa Tanzania na Zanzibar wameeleza hayo leo Jumapili katika mjadala uliendeshwa kwa mtandao na Watch Tanzania. Mjadala huo uliongozwa na Hezron Makundi na uliangazia uliangazia maana ya Royal Tour kwa maendeleo ya Tanzania na namna itakavyonufaika.

 

Wengine walioshiriki mjadala huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Maduhu Kazi.

 

Akichangia mjadala huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana amesema uzinduzi wa filamu hiyo utakwenda kuonesha taswira hali ya Tanzania sambamba na kuitangaza. Amesema sasa milango ya masuala ya utalii na uwekezaji katika sekta hiyo inakwenda kufunguka zaidi.

 

“Namshukuru Rais Samia kwa maono makubwa ambayo kimsingi yamekuja wakati muafaka. Wizara ya Maliasili na Utalii tunamshukuru Rais Samia kwa sababu Royal Tour inakwenda kuitangaza Tanzania.

 

“Watu wengine wanaweza wasielewe Tanzania kuna vivutio vingi vya utalii, lakini sio wote wanavijua na utalii unachangia pato la Taifa kwa asilimia 17. Kuna hifadhi za Taifa 22, lakini mtu anaweza kuzijua za Ngorongoro, Serengeti na Mikumi, sasa Royal Tour itaelezea haya yote kwa jamii ya kitaifa na kimataifa,”amesema Dk Chana.

 

Mbali na hilo, Dk Chana amesema Tanzania kuna  game reserves 27, mapori tengefu yasiyopungua 42 na kilomita za fukwe zisizopungua 1428 akisema maene yote hayo yataelezwa vizuri ndani ya filamu ya Royal Tour.

 

Wakati Dk Chana akieleza hayo, Dk Abbas amesema Roya Tour ni filamu ya saa moja na dk 58 ikijumuisha matangazo na utangulizi na itakuwa ya lugha mbili Kiswahili na Kingereza. Amesema Rais Samia amekwenda maeneo mbalimbali ya vivutio na kueleza umuhimu wake huku akibainisha kuwa Tanzania ni Taifa la tisa kushiriki programu kama hiyo.

 

 “Malengo ya filamu hii kuitangaza Tanzania duniani sio Marekani pekee bali ili kuwavutia watu katika sekta za utalii, biashara na sanaa, viwanda kuitembelea, ndio maana uchukuaji wake umezingatia ubora wa kimataifa. Naamini itakuwa na mvuto katika kuwaleta watu wa dunia katika nchi yetu,” 

 

“Kesho itazinduliwa katika ukumbi wa makumbusho ya kihistoria New York jioni ikiangazia zaidi watu wa mashuhuri wa biashara, burudani na utalii. Lakini Aprili 21 itazinduliwa Los Angeles kwa kundi kubwa zaidi na itaangazia watu wa burudani na utalii zaidi,” amesema Dk Abbas.

 

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Simai Said amesema Royal Tour haijalenga soko la Marekani pekee yake bali itakwenda mbali hasa kupitia mtandao. Amesema Royal Tour pia tasaidai watu wa Marekani kuijua Tanzania na Zanzibar.

 

“Sasa kama nchi tujipange namna ya kutoa huduma zetu kuingia hadi kutoka kwa wageni iwe wameingilia Kilimanjaro, Zanzibar, Dar es Salaam tunahakikishe huduma zetu zinakuwa za viwango. Tuhakikishe mnyororo wa thamani wote wa huduma anayoipata mtalii uandane na hadhi ya sura ya nchi,” amesema Simai.

 

Mkuregenzi wa Mkuu Kituo cha Uwezekazji Tanzania (TIC), Dk Maduhu Kazi amesema taasisi yake imejiaanda vema kwa fursa itakayotokana na Royal Tour, akisema ndani siku chache zijazo kutaingiwa mikataba ya makubaliano kati ya kampuni za Marekani na Tanzania.

 

“Kwa ile michakato iliyokamilika, tumeona kutakuwa na uwekezaji mkubwa, unaokuja Tanzania. Muda wa kamili wa kutaja miradi na thamani bado haujafika, lakini niwaeleze kutakuwa na manufaa makubwa,” amesema Dk Kazi.