BOT yaainisha sababu kukua uchumi 2023

BOT yaainisha sababu kukua uchumi 2023

General / 1st February, 2023

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imesema katika kipindi cha mwaka huu uchumi unatarajiwa kuimarika zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Hayo yamesemwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, katika taarifa yake iliyowekwa kwenye tovuti ya BoT jana.

Tutuba alisema Kamati ya Sera ya Fedha ilikutana juzi kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha, mwenendo wa uchumi na mwelekeo wa sera ya fedha na kubaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka jana ulikuwa na mafanikio.

Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kiwango cha ukwasi kuwa cha kutosha kwenye uchumi na mikopo kwa sekta binafsi ikiendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu cha takribani asilimia 21.

Sambamba na hilo, alisema kamati ilibaini kuwa mwenendo wa uchumi kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ulikuwa wa kuridhisha katika kipindi cha robo tatu za kwanza za mwaka jana ambapo uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka juzi.

Alisema ukuaji huo ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, ujenzi na uzalishaji viwandani wakati kwa upande wa Zanzibar uchumi ulikua kwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na asilimia 5.8 na ukichangiwa zaidi na shughuli za malazi na chakula, ujenzi, viwanda na upangishaji majengo.

Kutokana na mwenendo huo, Tutuba alisema katika kipindi cha mwaka huu, uchumi unatarajiwa kuimarika zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

“Uwekezaji wa Serikali kwenye sekta za uzalishaji na miradi ya kimkakati, kuimarika kwa shughuli za utalii pamoja na mazingira ya biashara na sera wezeshi za fedha na bajeti, vilevile kuimarika kwa mnyororo wa ugavi duniani kutachangia ukuaji huu,” alisema Tutuba.

Hata hivyo, kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi na matarajio katika nusu ya pili ya mwaka 2022/23, Kamati iliridhia BoT iendelee kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi kwa Januari na Februari mwaka huu. Uamuzi huo umetajwa kulenga kukabili ongezeko la mfumuko wa bei na kuchochea kuimarika kwa shughuli za uchumi nchini.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda, alisema kiwango cha ukwasi kuwa cha kutosha kwenye uchumi ina maana ujazo wa fedha kwenye mzunguko ni wa kutosha.

Mwang’onda alisema kiwango cha kutosha cha fedha kwenye mzunguko kinaweza kuchangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya serikali kwenye miradi ya kimkakati, misamaha ya kodi na watu kutofungiwa biashara zao.

Pia alisema kunapokuwa na fedha za kutosha kwenye mzunguko ina faida kiuchumi kwa kuwa inapunguza riba za mikopo na kufanya watu wengi kukopa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na biashara.

Kwa kuwa taarifa hiyo ya BoT ilibainisha kuwa mikopo kwa sekta binafsi nayo ikiendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu cha takribani asilimia 21, Mwang’onda alisema itasaidia kuwatoa watu katika umasikini.

“Kuwa na ukwasi wa kutosha katika uchumi ni muhimu kwa sababu unachechemua uchumi, benki zitakuwa na uwezo wa kukopesha zaidi kwa kuwa huwezi kuendesha uchumi kama mabenki hayapo imara na mikopo kwa wajasiriamali haitakuwepo,” alisema Mwang’onda.